Wakati siku zikiendelea kusonga taratibu mabadiliko ya kiteknolojia nayo yanazidi kushika kasi nchini na duniani kwa ujumla hali ambayo inawataka waandishi wa habari kujifunza na kutumia mbinu za kisasa na za kidijitali katika kazi zao.

Katika kuhakikisha hilo wadau mbali mbali wa sekta ya habari nchini wamekua wakiandaa programu mbali mbali ambazo zinalenga zaidi kuwasaidia waandishi kupata ujuzi na kuweza kutumia mbinu mbali mbali za kidijitali ili kuweza kuambatana na hali ya teknolojia inavyoendelea duniani kote.

Miongoni mwa taasisi zinazofanya juhudi za kuwaelimisha wanahabari juu ya mbinu za kidijitali pamoja na umuhimu wa kuzitumia katika kazi zao ni pamoja na Kampuni ya Media Covergency ya Tanzania wakishirikiana na Internews kupitia mradi wao wa Women at Web. Katika mradi huo wamelenga zaidi kuwaelimisha waandishi wa habari wanawake nchini juu ya uandishi wa habari wa kidijitali.

Katika utoaji wao wa elimu hizo wamekua pia wakiwaelimisha waandishi hao juu ya namna mbali mbali za kuweza kujiajiri katika taaluma zao kwa kutumia simu janja kwa namna mbali mbali kama vile kupitia mitandao ya kijamii na kadhalika. Mbali na kuwaelimisha waandishi hao kumekua na changamoto mbali mbali ambazo hujitokeza kwa waandishi wa habari wenyewe lakini pia changamoto ambazo hata waandaaji wa programu hizo hukutana nazo wakiwa katika safari ya kuhakikisha waandishi wa habari wanaendana na kasi ya teknolojia. 

Mkurugenzi (CEO) wa kampuni ya Tech & Media Convergency Bi. Asha D Abinallah, amesema kuwa miongoni mwa changamoto anazokumbana nazo yeye kama kiongozi katika uelimishaji ni pamoja na kwamba wengi wanakubali kupata elimu lakini wachache ndio wanafanya yale waliyoelekezwa. “Waandishi wengi sana wanapokuja kupokea mafunzo huwa wanakuja na mtazamo wa kupata vocha tu na sio kupata elimu” alisema Bi. Abinallah

Alisema kuwa hali ya waandishi kujali fedha katika mafunzo na sio kile wanachofundishwa ni miongoni mwa changamoto ambazo bado wanakumbana nayo kwa kiasi kikubwa hali ambayo inapelekea waandishi kupoteza thamani yao na thamani ya taaluma yao kwa ujumla.

Bi. Abinallah amewaomba na kuwashauri waandishi kubadili mitazamo yao na kuelekeza nguvu nyingi sana katika kuambatana na teknolojia na uandishi wa habari wa kidijitali kwani teknolojia haikwepeki.

“Mimi ninasihi kwelikweli kwamba kuweza kubadilika kwa muandishi na kwenda na hii kasi ya kidigitali inabidi yeye mwenyewe akubali na aone na alewe mantiki na thamani” amesema Bi. Abinallah

Alisema kuwa muandishi wa habari anatakiwa asome na ajifunze ili aweze kuona na kujifunza ni nini kinaendelea katika hii dunia ya leo. Mbali na changamoto wanazokutana nazo waandaaji wa programu mbali mbali pia kuna changamoto nyingi ambazo waandishi wa habari wanapitia na zinawazuia wao kufukuzana na kasi ya teknolojia katika taaluma yao.

Miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo waandishi ni pamoja na muda, waandishi wengi huwa wanatamani mafunzo yawe kwa muda mrefu kutokana na kwamba mara nyingi mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa siku chache tu. Lakini pia changamoto nyingine ambayo wanakumbana nayo  ni kukosekana kwa nyenzo ambazo wao wanaweza kutumia katika kuufanya uandishi wa habari wa kisasa zaidi. Waandishi wengi huwa hawafaahamu wapi wataanzia katika kujiendeleza na kukabiliana na teknolojia katika taaluma yao ili wasibaki nyuma na waweze kusonga mbele zaidi.

Hata hivyo,Bi. Abinallah alizungumzia juu ya matokeo wanayopata baada ya kuwafundisha waandishi na amesema kuwa katika mafunzo wanayoyatoa huwa wanapata matokeo mazuri na chanya na hiyo ni kutokana na wao kuelewa changamoto wanazopitia waandishi na wao hutumia nafasi hiyo kuwasaidia waandishi kutatua changamoto zao kwa kuwapatia elimu na maarifa.

“Wapo waandishi wengi ambao wamepata elimu kutokana na programu zetu na wanafanya vizuri sana katika mitandao ya kijamii na wanaonekana” amesema Bi. Abinallah

MARIA ACLEY | NUKTA AFRICA

DIGITAL JPOURNALISTS 2021/22

BORESHA HABARI PROJECT

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *