Uandishi wa habari ulianza miaka mingi ya nyuma ambapo watu waliwasiliana kwa kutumia pembe za wanyama na ngoma ili kuita watu wajumuike pamoja na taarifa lengwa kutolewa, hio ilikua ni njia ya mwanzo kabisa ya mawasiliano, ambapo baadae ugunduzi wa magazeti ulitokea hivyo watu walipata taarifa kupitia magazeti na baada ya hapo vyombo vingine vya habari vikaendelea kugundulika ikiwemo redio, televisheni pamoja na mitandao ya kijamii.

Lakini kila baada ya ugunduzi wa chombo kingine cha habari chombo cha nyuma kinaonekana kua na hadhira pungufu tofauti na ilivyokua mwanzo, mfano usomaji wa magazeti umepungua kwa watu wengi kutonunua nakala za magazeti ili kujisomea, katika nakala yake ya ” The Present and Future of Journalism: How News Media Lost It’s Purpose” by Martin Gurri ameandika Kua katika nchi za umoja wa wilaya magazeti 2000 yalifungiwa tangu mwaka 2004, lakini pia ajira kwenye vyombo vya habari vilipungua kwa 57% tangu 2008 na zaidi ya wanahabari 16,000 walipoteza kazi zao kwa mwaka 2020 pekee.

Kwa maana hiyo wanahabari wanapaswa kua na mbinu mbali mbali za kujikita katika kujiajiri katika uandishi wa habari wa kidijitali ili kuweza kujipatia ajira pamoja na kufufua njia nyingine za habari ambazo zinaonekana kuzidi kudidimia kwa kupungukiwa na hadhira yake. “Reuters Institute 2021 Digital News report” katika kitabu chake ameandika kua zaidi ya 40% ya watu chini ya miaka 35 wanafuatilia zaidi habari za mitandaoni, hivyo wanahabari pia wanapaswa kua na ujuzi zaidi wa matumizi ya mitandao mbalimbali ya kijamii na njia za kidijitali ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na kukuza uandishi wa habari.

Njia za kidijitali ni muhimu na ni nzuri katika kufikia jamii yenye watu wengi hasa Vijana ambao wapo kidijitali zaidi,  lakini njia hizi za kidijitali zisiposimamiwa kwa umakini vinapotosha umma kwa kiasi kikubwa kwani watu wengi wanaamini katika mitandao ya kijamii, mfano hivi sasa kila mtu hata asiye na vigezo vya kuandika habari anaweza kuandika habari potofu mitandaoni na kupotosha umma, zipo kurasa nyingi za Instagram na mitandao ya YouTube nk ambazo huchapisha habari potofu, hivyo uandishi wa kidijitali unahitaji usimamizi wa hali ya juu zaidi.

Ukuaji wa kidijitali umepelekea kuwepo kwa matangazo pamoja na taarifa nyingi potofu katika jamii, na pia kumekua na kugushi kwa mihuri pamoja na sahihi za watu mbali mbali ili kutoa taarifa za uongo.

Lakini pia ili tuwe na waandishi mahiri wenye kuikosoa jamii na kuleta maendeleo ya taifa, ni muhimu kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari pamoja na mzingira rafiki ya waandishi wa habari kufanya kazi zao, takwimu zilizotolewa na shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka (R.S.F), imetoa ripoti na kuonyesha kua Tanzania imeporomoka kwa nafasi 25 katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kati ya nchi zilizofanyiwa tathmini ambazo ni 180, na kuweka bayana mambo yaliyochangia kuporomoka huko ikiwa ni pamoja na kuvamiwa kwa clouds media group 2017, kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari, kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mwandishi wa kujitegemea Azory Gwanda nk.

Lakini pia katika mwaka wa 2018 takribani waandishi wa habari 95 wameuawa wakiwa kazini hii ni kwa mujibu wa (I.F.J). Hivyo uhuru wa vyombo vya habari na mazingira rafiki ya waandishi wa habari ya kufanyia majukumu yao itasaidia katika kuendeleza taifa katika nyanja tofauti tofauti kama kiuchumi, kisiasa, kimichezo, kiutamaduni, biashara nk.

ROSELINE SANGA | FREELANCER

DIGITAL JOURNALIST 2021/22

BORESHA HABARI PROJECT

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *