WAKATI dunia ikisonga mbele hususan katika kukua kiteknolojia wanawake hawajaachwa nyuma, ili kufikia mapinduzi ya maendeleo kidigitali. Wanawake wanahabari nchini wapatao 60 kutoka mikoa tofauti wamepewa mafunzo ya kukuza ujuzi kidigitali kupitia taaluma yao, ili kubaini fursa na namna ya kuandika habari zinazohusisha data, wamepatiwa ujuzi kupitia mpango wa Women At WebTZ, uliowezeshwa na Boresha Habari kupitia USAID Tanzania. Wakufunzi katika mafunzo hayo, Lily Urio, Zahara Tunda na Ashura Babi ambao kwa namna tofauti wanawasilisha mada tofauti kwa wanahabari ikiwamo kuandika taarifa za kidigitali na mbinu za kubadili fikra na kuegemea uandishi wa kidigitali.

Zahara Tunda anasema uandishi wa kidigitali huwa unakuwa na namna tofauti ikiwamo unaotumia michoro, picha na maimbo tofauti ili kumvutia msomaji katika makala au habari iliyochapishwa au kurushwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Badala ya kuandika namba kwenye habari yako, mwandishi unatakiwa kuwa mbunifu kwa kutumia vielelezo, michoro, ambavyo vinatafsirika haraka kwa msomaji. Mara nyingi watu huogopa namba zenye tarakimu nyingi, lakini ‘graph’ itasaidia kupunguza woga,” anasemaa Tunda.
Mkufunzi Lily anasema kila mwandishi anayetamani kuwa mwandishi wa kidigitali ni lazima awe na uwez mzuri wa mawasiliano, fikra pana na kuwa na wazo la kutoa suluhisho la haraka kupitia uandishi.
“Unaweza kujua nbamna ya kukusanya taarifa kutoka vyanzo mbalimbali hasa mitandao ya kijamii uwe nayo karibu kwa kufahamu kinachopendwa kwa wakati gani. Tambua namna bora na mbinu za uandishi wa data na kuhusisha habari zako mtandaoni kwa sababu ulimwengu ni kidigitali zaidi,” anasema Lily.

MPANGO ULIOPO

Mpango wa mradi wa Women At Web project unaosimamiwa na Tech & Media Convergency, umelenga kuhakikisha wanawake waliopo mijini na nje kidogo ya mji wananufaika na mabadiliko ya kidigitali,
Nchi zilizomo kwenye mradi huo ni Uganda, Kenya, Tanzania na Rwanda kwa lengo la kuwapa ujuzi wa kidigitali hususan wanawake vijana ambao watafanikiwa kukabiliana na ukatili wa kijinsia mtandaoni kwa kutoa taarifa mbalimbali.
Mitandao ya kijamii, hivi sasa ina watumiaji wengi hasa kupitia instagram, facebook, whatsapp, YouTube, na mingineyo huku ikikadiriwa watumiaji wa huduma hiyo wanafikia bilioni 3.8  na kuwa kati ya mbinu mpya inayoifikia dunia kwa haraka zaidi.

WANAWAKE NA DIGITALI

Mkurugenzi Mtendaji wa Zaina Foundation, Zaituni Njovu akizungumza kwenye moja ya mafunzo ya wanahabari wanawake, yaliyolenga kuwaongezea ujuzi, ikiwamo kulinda vifaa vyao vya kazi pamoja na kuzingatia usahihi wa vyanzo vya habari, anasema wanawake wapo nyuma katika mapinduzi ya kiteknolojia.
Zaituni anasema lengo ni kuwawezesha wanawake kwa kuwapa ujuzi wa namna ya kuhakikisha usalama katika matumizi ya mtandaoni kwenye dunia ya kidigitali, ikizingatiwa kundi ni kubwa la wanawake ambao bado halijajihusisha na Teknolojia Mawasiliano (IT).
“Haki ya kupokea, kutuma, kutoa taarifa ni ya kila mmoja. Lakini tunahitaji kuwepo usalama wa matumizi ya mtandao, kulindwa kwa faragha, kwa kuwa wanawake ni kati ya waathiriwa wakubwa wa picha zisizo na maadili zikisambazwa mitandaoni bila mtu kujua,” anasema Zaituni.
Anasema mteja anayejiunga na huduma za mtandao ana haki ya kulindwa usalama wake, kupata huduma ya uhakika bila kukatika na iwapo inatokea tatizo la kiufundi, taarifa itolewe kwa mtumiaji.
“Mtumiaji ameamua kujiunga na kifurushi cha siku au hata wiki, lakini baada ya muda unaambiwa mtandao wa kampuni fulani haupatikani bila taarifa yeyote. Ni haki yako kupata taarifa, wakati wowote,” anasema Zaituni.
Anafafanua kwamba mafunzo hayo ambayo ni ya awali kutolewa kwa wanahabari, yanawaongezea ujuzi wanahabari, ili kukabiiana na changamoto zilizopo mtandaoni pamoja na kujiongezea fursa za kiuchumi.12:00

“Tunawaelimisha wanawake katika matumizi ya teknolojia na mtandao, wakati matumizi ya teknolojia yakikua ipo haja ya kuwa makini na matumizi ikiwamo kuvamiwa kimtandao na kuvujisha siri zako, ikizingatiwa tunaelekea kwenye uchaguz mkuu inabidi kuwa makini,” anasema Zaituni.
IDADI YA WATUMIAJI
Zaituni anasema hivi sasa takwimu duniani zinaonyesha watumiaji wa mtandao (intaneti), imeongezeka na kufikia watu bilioni 4.5 duniani na kati yao watumiaji milioni 23 ni kutoka Tanzania. “Wakati matumizi yakikua dunia ni muda wa kuongeza usalama ya kimtandao kwa mtumiaji, wadau kwa kuwawezesha namna ya kuweka usiri wa taarifa zao na data zao,” anasema Zaituni.
CHANGAMOTO MTANDAONI 

Zaituni anasema zilizopo katika mtandao ni usalama mdogo huku wanawake kadhaa wakiwa na elimu ndogo.
“Changamoto ni elimu kwa ambao wanatakiwa kufikisha habari kupitia mtandao, ili kutoa taarifa sahihi kuelimisha umma kipindi amcho ulimwengu tunahitaji elimu zaidi,” anasema.

Zaituni anasema kutokana na watu wengi kuwa na elimu ndogo ya kulinda taarifa, picha zao imekuwa ni kawaida kuona picha za kuwadhalilisha hasa wanawake zikisambaa maeneo tofauti bila wao kujua,” anaeleza Zaituni.

https://www.ippmedia.com/sw/makala/wanawake-wanahabari-katika-mbinu-mpya-uandishi-kidigitali

IMEANDALIWA NA CHRISTINA MWAKANGALE | IPP MEDIA

MWANDISHI WA KIDIJITALI 2021/22

BORESHA HABARI PROJECT

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *